Wednesday, November 18, 2009

Chuo Kikuu IMTU chasitisha masomo ya udaktari wa meno

Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Udaktari na Teknolojia (IMTU), kimesitisha utoaji wa shahada ya udaktari wa meno (DDS) katika kipindi kisichojulikana kuanzia mwaka uliopita.


Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Shija, amewaambia waandishi wa habari kuwa masomo hayo yalisimamishwa tangu mwaka uliopita, ikiwa ni baada ya mabadiliko ya uongozi wa kitaaluma chuoni hapo.

Aidha, akasema kusimamishwa kwa shahada hiyo kunatokana na gharama za uendeshaji wa masomo hayo kuwa kubwa, idadi ndogo ya wadahiliwa na kuwepo kwa mhadhiri mmoja pekee chuoni hapo .

“Baada ya kuingia kwa uongozi mpya wa kitaaluma, tulifanya marekebisho ya uendeshaji na kuamua kusimamisha kwanza shahada ya madaktari wa meno,” akasema Profesa Shija.

Akasema ulipoingia uongozi mpya ulikuta wanafunzi walioomba kudahiliwa katika kozi hiyo ni 10 pekee, idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na gharama za uendeshaji wa masomo katika fani hiyo.

Katika hatua nyingine, amesema idadi ya wadahiliwa katika chuo hicho imeongezeka kutoka jumla ya wadahiliwa 500 katika kipindi cha mwaka juzi hadi kufikia 900 Oktoba mwaka huu.

Akasema mafanikio hayo yametokana na uongozi mpya wa kitaaluma uliochukua nafasi za uongozi mwaka jana ambapo mchakato wa uendeshaji wa chuo hicho ulifanyiwa marekebisho.

“Awali katika masomo ya udaktari wanafunzi walikuwa wakisoma kwa muda wa miaka minne na nusu... lakini baada ya kuja kwa uongozi mpya, tumebadilisha na kuwa miaka mitano na hivyo kuendana na vyuo vingine vya udaktari ulimwenguni,” akasema.

Akasema kati ya wanafunzi hao waliodahiliwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wa Kitanzania tofauti na miaka ya nyuma ambapo Watanzania walikuwa hawazidi watano.

Akitoa mfano, akasema mwaka jana pekee, Watanzania waliohitimu walikuwa ni wawili , ilhali idadi kubwa ikibakia kuwa ya raia wa India ambao baada ya kumaliza masomo yao chuoni hapo, walirudi kufanya kazi nchini kwao India.

Akasema tangu uongozi huo uanze kazi mwanzoni mwa mwaka jana, idadi ya wadahiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

No comments: