Monday, September 28, 2009

madenti hawa vipi?

Masela watatu, akiwamo denti wa kidato cha sita katika Skonga ya Sekondari ya Azania, wamenaswa wakiwafanyia (paper) mitihani wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).Frank Kaduma, aliyekuwa anamfanyia mtihani mwanafunzi aliyemtaja kwa jina moja la Tina, alikuwa ameahidiwa na mtu aliyemuunganisha na mtahiniwa huyo kuwa baada ya kutoka kwenye mtihani huo angelipwa sh 150,000.


Kwa mujibu wa Msajili wa Wanafunzi chuoni hapo,kitambulisho alichokuwa akikitumia Frank kumfanyia Tina mtihani kilikuwa na jina la Christian Mbago, mwanafunzi wa mwaka wa tatu.Akijieleza mara baada ya kunaswa Frank alisema kuwa...aliitwa na rafiki yake ambaye hata hivyo hakutaka kumtaja jina, na baadaye alimuunganisha na mtahiniwa na kukubaliana kiasi hicho cha fedha baada ya kazi hiyo kumalizika.“Mimi ninasoma Azania, nachukua PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati), rafiki yangu anasoma masomo ya biashara na mtihani wa leo una hisabati, hivyo juzi nilikuja naye ili anionyeshe darasa na leo ndiyo nimekuja kumfanyia mtihani,” alisema Kaduma.

Wakati mwanafunzi huyo akihojiwa, mwanafunzi mwingine, John Kapinga, alikamatwa na kupelekwa katika ofisi ya msajili baada ya kukutwa akimfanyia mtihani mwanafunzi wa mwaka wa tatu chuoni hapo, Joel Mlengule, anayesoma Stashahada ya Juu ya Hifadhi ya Jamii (Advanced Diploma in Social Protection).

Kapinga, alikiri kuwa alihitimu kidato cha sita mwaka 2003, akisoma masomo ya PCM, pamoja na kuahidi kwamba angetoa ushirikiano ili kumkamata mtahiniwa halisi.“Sikutaka kufanya, ila nilishawishiwa mara nne sikutaka, hata ikafikia hatua ndugu yake kunishawishi, nikakubali, ila dhamiri ikinisuta. kwani hakuna malipo yoyote tuliyoahidiana na ndugu yangu huyo,” alisema Kapinga huku akijiinamia.Chanzo chetu kilishuhudia kitambulisho chake kikiwa na jina la Joel Mlengule, kikiwa na namba ya usajili ADSP/16492/2007 na kinamalizika muda wake mwaka huu.Kwa upande wake, Joel Mlengule, aliyefanyiwa mtihani na kukamatwa akiwa nje ya eneo la IFM akimsubiri Kapinga, alinaswa na walinzi wa chuo na kuhojiwa, ambapo alikiri kufanyiwa mtihani na Kapinga.

Mlengule ambaye ni mkazi wa Upanga, jijini Dar es Salaam, alikiri kuwapo mtu aliyemuunganisha na Kapinga, baada ya kufeli somo lake la hesabu mara mbili mfululizo, hivyo hakutaka hali hiyo imrudie, hasa ikizingatiwa kuwa huo ulikuwa mtihani wa mwisho chuoni hapo.“Ni kweli alikuwa ananifanyia mtihani baada ya kufeli somo hili mara mbili. Niliona mwaka huu, na huu ni mtihani wangu wa mwisho, mimi sijui hesabu, ndiyo maana hata aliponiambia anifundishe nilikataa na kumwomba anisaidie kunifanyia,” alisema Mlengule.

Kwa mujibu wa Msajili wa Wanafunzi chuoni hapo, tukio jingine la namna hiyo lilitokea hivi karibuni, ambapo msichana mmoja alikimbia na kuacha viatu vyake, baada ya kubainika kuwa alikuwa akimfanyia mtihani mwanafunzi ambaye jina lake halikupatikana mara moja.Aliongeza kuwa, mwaka jana matukio hayo yalitokea na imebainika kuwa kuna wakala anayewaunganisha wanafunzi wa chuo na watu wa nje kuwafanyia mitihani hiyo kinyume cha taratibu.
 
ninajiuliza tutafika kweli hivi?kwa kweli hii ni hatari kwa maendeleo ya nchi yetu,toa maoni yako by mwandishi.

No comments: