Tuesday, December 8, 2009

Polisi wawakabili raia kwa risasi

Polisi wilayani Rorya mkoa wa Mara, wamefyatua risasi za moto katikati ya raia na kuua watu wawili na kuwajeruhi wengine tisa. Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwani wakati tunakwenda mitamboni habari zilionyesha kwamba baadhi ya majeruhi walikuwa na hali mbaya.
Waliokufa katika tukio hilo, wamejulikana kuwa ni Iranda Matoka (26) na Abbas Adek (23). 
Aidha, majeruhi walitajwa kwa majina ya Wandiba Nyamkondya (26), Julius Nduku (26), Aziz Mganga (18), Sanga Matiko (32), Isiro Magesa (38), Ezekiel Robert (15), Ramadhani Magige (32), Musoba Rhobhi (32) na Leonard Kahanga.
Tukio hilo lilitokea jana, wakati askari hao walipokabiliana na wakazi wa kijiji cha Moharango, walioandamana kwenda kituo cha polisi Utegi, wakitaka kuachiwa huru kwa wazee wanne wa mila.

Wazee hao waliojulikana kwa majina ya Kahanga Mwando, Odila Runyola, Saba Kahanga na Wasaga Mganga, walikamatwa kwa madai ya kutishia kumroga na kumuua mkazi wa kijiji hicho, Joseph Ngondi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Nipashe, madai ya kumroga na kumuua Ngondi, yalitokana na hatua ya mwanakijiji huyo kufyeka mlima Nyabigiga, unaosadikiwa kutumika kwa masuala ya tambiko.

Watu walioshuhudia tukio hilo, waliliambia Nipashe kuwa baada ya wazee hao kukamatwa na kuwekwa ndani juzi, wanakijiji hao waliandama kwenda kituoni hapo kwa lengo linalodhaniwa kushinikiza kuachiwa kwa wazee wa kijiji, ndipo walipokabiliana na polisi waliokuwa na silaha zenye risasi za moto.
``Tulisikia milio ya risasi na baadaye vilio huku watu wakikimbia hovyo,`` mmoja wa mashuhuda ambaye jina lake halikupatikana, alisema.
Miili ya watu waliokufa na majeruhi ilipelekwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime.

Majeruhi katika tukio hilo, miongoni mwao wakiwa katika hali mbaya, walijeruhiwa mikononi, miguuni, mgongoni na mapajani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow, hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.
 "hawa vipi jamani? unayaamini haya wanayoyafanya?toa maoni yako".

Wednesday, November 18, 2009

Chuo Kikuu IMTU chasitisha masomo ya udaktari wa meno

Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Udaktari na Teknolojia (IMTU), kimesitisha utoaji wa shahada ya udaktari wa meno (DDS) katika kipindi kisichojulikana kuanzia mwaka uliopita.


Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Shija, amewaambia waandishi wa habari kuwa masomo hayo yalisimamishwa tangu mwaka uliopita, ikiwa ni baada ya mabadiliko ya uongozi wa kitaaluma chuoni hapo.

Aidha, akasema kusimamishwa kwa shahada hiyo kunatokana na gharama za uendeshaji wa masomo hayo kuwa kubwa, idadi ndogo ya wadahiliwa na kuwepo kwa mhadhiri mmoja pekee chuoni hapo .

“Baada ya kuingia kwa uongozi mpya wa kitaaluma, tulifanya marekebisho ya uendeshaji na kuamua kusimamisha kwanza shahada ya madaktari wa meno,” akasema Profesa Shija.

Akasema ulipoingia uongozi mpya ulikuta wanafunzi walioomba kudahiliwa katika kozi hiyo ni 10 pekee, idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na gharama za uendeshaji wa masomo katika fani hiyo.

Katika hatua nyingine, amesema idadi ya wadahiliwa katika chuo hicho imeongezeka kutoka jumla ya wadahiliwa 500 katika kipindi cha mwaka juzi hadi kufikia 900 Oktoba mwaka huu.

Akasema mafanikio hayo yametokana na uongozi mpya wa kitaaluma uliochukua nafasi za uongozi mwaka jana ambapo mchakato wa uendeshaji wa chuo hicho ulifanyiwa marekebisho.

“Awali katika masomo ya udaktari wanafunzi walikuwa wakisoma kwa muda wa miaka minne na nusu... lakini baada ya kuja kwa uongozi mpya, tumebadilisha na kuwa miaka mitano na hivyo kuendana na vyuo vingine vya udaktari ulimwenguni,” akasema.

Akasema kati ya wanafunzi hao waliodahiliwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wa Kitanzania tofauti na miaka ya nyuma ambapo Watanzania walikuwa hawazidi watano.

Akitoa mfano, akasema mwaka jana pekee, Watanzania waliohitimu walikuwa ni wawili , ilhali idadi kubwa ikibakia kuwa ya raia wa India ambao baada ya kumaliza masomo yao chuoni hapo, walirudi kufanya kazi nchini kwao India.

Akasema tangu uongozi huo uanze kazi mwanzoni mwa mwaka jana, idadi ya wadahiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Tuesday, November 3, 2009

hii sheria vipi?Auawa Dar kwa tuhuma za wizi

Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni kibaka ameuawa kwa kupigwa kwa mawe na wananchi wenye hasira kali baada ya kudaiwa kukutwa akiezua mabati katika nyumba iliyokuwa ikiendelea kujengwa.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mark Kalunguyeye amesema tukio hilo limetokea jana saa 3:30 usiku Kimara Stop Over , Jijini Dar es Salaam.
Akasema marehemu akiwa na wenzake watatu walifika katika nyumba hiyo inayomilikiwa na Bathelomeo Kijazi na kuanza kuezua mabati hayo kwa lengo la kuyaiba.
Hata hivyo, akasema wakati wakiendelea na uezuaji huo, majirani walisikia na kuanza kupiga kelele zilizowashtua watu wengine na kuanza kuwafuatilia.
“Waliposikia kelele, vibaka hao waliamua kushuka huku kila mmoja akabeba bati lake na kuanza kukimbia,”akasema.
Akasema wananchi walianza kuwafukuza na kufanikiwa kumkamata kibaka mmoja.
Kamanda huyo akasema baada ya kumkamata wananchi hao walimshambulia kwa mawe ambapo jiwe moja lilimpata kisogoni na kudondoka chini.
Akasema mtu huyo alifariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya matibabu.
Akasema katika tukio hilo vibaka hao walifanikiwa kuondoka na mabati matatu na kuongeza uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kuwakamata vibaka waliokimbia,
mambo vipi haya?toa maoni!!!!

Thursday, October 29, 2009

ulipuaji bomu wauwa dar

Watu wawili wamezirai baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana kufanya zoezi la kulipua mabomu katika kambi yake iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam.

Waliozirai katika tukio hilo la ulipuaji mabomu ni Rosemary Tarimo na aliyetambulika kwa jina la Matilda, ambao walikimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Uamuzi wa Jeshi hilo kulipua mabomu yake unatokana na silaha hizo kulipuka zenyewe katika kambi ya Mbagala na kusababisha watu zaidi ya 20 katika eneo hilo kufariki dunia.
Zoezi hilo lilifanyika jana kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 11:00 jioni ambapo kabla ya kufanya shughuli hiyo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Husein Mwinyi alitoa tahadhari kwa wananchi kukaa mbali wakati ulipuaji huo ukifanyika.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi alisema, licha ya taarifa kutolewa mapema kwa vyombo vya habari, ulipuaji wa mabomu hayo ulisababisha shughuli mbalimbali kusimama ikiwemo watu kufunga maduka yao na wengine kuhama nyumba kwa kuhofia kupoteza maisha yao.
Lukuvi alisema shughuli za ugawaji wa chakula katika kambi maalumu iliyojengwa kwa ajili ya kuwahifadhi watu walioathiriwa na mabomu yaliyolipuka yenyewe hivi karibuni nao ulisimama.
Aidha, Lukuvi alisema shughuli za kutathmini uharibifu wa mali uliotokana na mabomu hayo haujakamilika kutokana na ukosefu wa watalaamu kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Aliwaomba watu wenye ujuzi wa kufanya tathmini ya uharibifu wa mali kujitokeza haraka ili waweze kusaidia kujua thamani halisi.
Vilevile, Mkuu huyo wa mkoa alisema watu 14 bado wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kuathiriwa na mabomu hayo yaliyolipuka huko Mbagala hivi karibuni.
Alisema mmoja wa watu hao hali yake ni mbaya na amelazwa chumba cha watu mahututi (ICU) katika hopitali hiyo.
Baada ya kutokea ajali hiyo watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara walianza kumimina misaada kwa wahanga ili kuwawezesha kujikimu baada ya baadhi yao kupoteza mali zao zikiwemo nyumba.
Zoezi la ilipuaji mabomu hayo jana lilishuhudiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali, Davis Mwamunyange.
"nibudi wananchi kulindwa na majanga yanayoweza kuepukwa".

Thursday, October 22, 2009

RAGE BADO YUMO!!!!! Simba wamtaka Rage kutowabeep

Wanachama wa klabu ya Simba wamemtaka Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Tanzaniai, FAT (sasa TFF), Ismail Aden Rage, aliyetangaza nia ya kuwania uenyekiti katika klabu hiyo 'kutowa-beep' bali agombee kweli.

Pia wanachama hao, wamesema wapo tayari kumpa nafasi hiyo Rage kutokana na wasifu wake katika soka na hususani klabu yao na hivyo wanamtaka ajitose kweli na sio kutishia toto tu.
Wakizungumza na Nipashe jana, baadhi ya wanachama hao, wakiwemo wazee walisema wamefurahishwa na taarifa kwamba Rage anataka kujitosa kwenye kinyang;anyiro cha uchaguzi mkuu ujao wa Simba, ila hawana hakika.
Mmoja wa wanachama na wazee wa klabu hiyo, Mzee Juma Hulungu, alisema kama ni kweli Rage ana nia ya kuwania uongozi Simba wanamkaribisha na kumhakikishia kuwa wanachama watampa nafasi atakayoiomba.
Hulungu, alisema hakuna wanachama wa Simba asiyemjua Rage na utendaji wake makini na jinsi alivyoisaidia mno klabu yao na hivyo ni muhimu ajitose ili wampe nafasi hiyo kuwaletea mafanikio na maendeleo.

Mwanachama mwingine 'kigogo' alisema kwa ufupi kwamba, kama ni kweli Rage anataka nafasi hiyo ajitokeze na wala asiwatie hamu wanachama kwani klabu yao inahitaji watu kama wao katika kuikwamua kimaendeleo.
Asitubeep, kama kweli anataitaka nafasi hii ajitokeze na hatutamuangusha, kwani tunathamini mchango na utendaji wake katika soka," alisema 'kigogo' huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Rage ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Tabora, alinukuliwa wiki iliyopita akisema ana dhamira ya kuwania Uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa Simba utakaofanyika Desemba mwaka huu.

Kiongozi huyo anakuwa ni wa pili kutangaza kuwania nafasi hiyo, kwani tayari mwanachama mwingine wa Simba, Bossy Matola alishatangaza dhamira ya kurithi nafasi hiyo inayoshikiliwa na Hassani Dalali.

Wednesday, October 21, 2009

washa moto kikwete"wabongo tunakuaminia"

Kuna taarifa kuwa baadhi ya vigogo Serikalini wameanza kujawa hofu na kuhaha huku na huko kutokana na hofu ya kupigwa chini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Kikwete, chanzo kikidaiwa kuwa ni fagio lake aliloanza kulipitisha kiaina katika kila eneo.

Aidha, hofu ya baadhi ya vigogo hao inadaiwa kutiwa nguvu na tetesi kuwa Rais anaendelea kuwang'oa kiujanja wale wote wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali yaliyoligharimu taifa.
Hadi sasa kuna mchakato wa kuisafisha Serikali kwa kuwawajibisha wale ambao utendaji kazi wao hauridhishi na pia wale wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali, chanzo kimoja kutoka Serikalini kimesema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya taarifa ya Rais kufanya mabadiliko katika safu ya Makatibu Wakuu na kuteua Mwanasheria mpya wa Serikali juzi na jana, hali imeendeea kuwa tete kwenye baadhi ya ofisi.
"Haya mabadiliko yaliyotangazwa juzi na jana yamekuwa tishio kwa baadhi ya vigogo... wengine wameanza kuhaha kutokana na hofu kuwa pengine nao watakumbwa na fagio la kuwatema kwa sababu mbalimbali," kikadai chanzo hicho.
Aidha, kikaongeza kuwa hivi sasa, baadhi ya vigogo wamekuwa hawatulii maofisini kwani muda mwingi wamekuwa wakinusanusa taarifa toka Ikulu juu ya kusikia kama kuna badiliko lolote.
Juzi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya makatibu wakuu wa baadhi ya Wizara, ambapo wengine waliachia ngazi kutokana na maelezo kuwa muda wao wa kusitaafu kwa lazima umewadia ilhali wengine wakihamishwa toka wizara moja hadi nyingine.
Aidha, jana Rais Kikwete alimteua Jaji Fredirick Mwita Werema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akichukua nafasi ya Johnson Mwanyika ambaye anastaafu.
Hata hivyo, Mwanyika ni miongoni mwa vigogo ambao Bunge lilitaka wawajibishwe kwa tuhuma za kuhusika kwao na kashfa ya kampuni tata ya umeme ya Richmond, kama ilivyo kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, ambaye naye ameondolewa nafasi hiyo na Rais kwa maelezo kuwa anakwenda likizo ya kustaafu.