Thursday, October 22, 2009

RAGE BADO YUMO!!!!! Simba wamtaka Rage kutowabeep

Wanachama wa klabu ya Simba wamemtaka Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Tanzaniai, FAT (sasa TFF), Ismail Aden Rage, aliyetangaza nia ya kuwania uenyekiti katika klabu hiyo 'kutowa-beep' bali agombee kweli.

Pia wanachama hao, wamesema wapo tayari kumpa nafasi hiyo Rage kutokana na wasifu wake katika soka na hususani klabu yao na hivyo wanamtaka ajitose kweli na sio kutishia toto tu.
Wakizungumza na Nipashe jana, baadhi ya wanachama hao, wakiwemo wazee walisema wamefurahishwa na taarifa kwamba Rage anataka kujitosa kwenye kinyang;anyiro cha uchaguzi mkuu ujao wa Simba, ila hawana hakika.
Mmoja wa wanachama na wazee wa klabu hiyo, Mzee Juma Hulungu, alisema kama ni kweli Rage ana nia ya kuwania uongozi Simba wanamkaribisha na kumhakikishia kuwa wanachama watampa nafasi atakayoiomba.
Hulungu, alisema hakuna wanachama wa Simba asiyemjua Rage na utendaji wake makini na jinsi alivyoisaidia mno klabu yao na hivyo ni muhimu ajitose ili wampe nafasi hiyo kuwaletea mafanikio na maendeleo.

Mwanachama mwingine 'kigogo' alisema kwa ufupi kwamba, kama ni kweli Rage anataka nafasi hiyo ajitokeze na wala asiwatie hamu wanachama kwani klabu yao inahitaji watu kama wao katika kuikwamua kimaendeleo.
Asitubeep, kama kweli anataitaka nafasi hii ajitokeze na hatutamuangusha, kwani tunathamini mchango na utendaji wake katika soka," alisema 'kigogo' huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Rage ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Tabora, alinukuliwa wiki iliyopita akisema ana dhamira ya kuwania Uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa Simba utakaofanyika Desemba mwaka huu.

Kiongozi huyo anakuwa ni wa pili kutangaza kuwania nafasi hiyo, kwani tayari mwanachama mwingine wa Simba, Bossy Matola alishatangaza dhamira ya kurithi nafasi hiyo inayoshikiliwa na Hassani Dalali.

No comments: