Wednesday, October 21, 2009

washa moto kikwete"wabongo tunakuaminia"

Kuna taarifa kuwa baadhi ya vigogo Serikalini wameanza kujawa hofu na kuhaha huku na huko kutokana na hofu ya kupigwa chini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Kikwete, chanzo kikidaiwa kuwa ni fagio lake aliloanza kulipitisha kiaina katika kila eneo.

Aidha, hofu ya baadhi ya vigogo hao inadaiwa kutiwa nguvu na tetesi kuwa Rais anaendelea kuwang'oa kiujanja wale wote wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali yaliyoligharimu taifa.
Hadi sasa kuna mchakato wa kuisafisha Serikali kwa kuwawajibisha wale ambao utendaji kazi wao hauridhishi na pia wale wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali, chanzo kimoja kutoka Serikalini kimesema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya taarifa ya Rais kufanya mabadiliko katika safu ya Makatibu Wakuu na kuteua Mwanasheria mpya wa Serikali juzi na jana, hali imeendeea kuwa tete kwenye baadhi ya ofisi.
"Haya mabadiliko yaliyotangazwa juzi na jana yamekuwa tishio kwa baadhi ya vigogo... wengine wameanza kuhaha kutokana na hofu kuwa pengine nao watakumbwa na fagio la kuwatema kwa sababu mbalimbali," kikadai chanzo hicho.
Aidha, kikaongeza kuwa hivi sasa, baadhi ya vigogo wamekuwa hawatulii maofisini kwani muda mwingi wamekuwa wakinusanusa taarifa toka Ikulu juu ya kusikia kama kuna badiliko lolote.
Juzi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya makatibu wakuu wa baadhi ya Wizara, ambapo wengine waliachia ngazi kutokana na maelezo kuwa muda wao wa kusitaafu kwa lazima umewadia ilhali wengine wakihamishwa toka wizara moja hadi nyingine.
Aidha, jana Rais Kikwete alimteua Jaji Fredirick Mwita Werema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akichukua nafasi ya Johnson Mwanyika ambaye anastaafu.
Hata hivyo, Mwanyika ni miongoni mwa vigogo ambao Bunge lilitaka wawajibishwe kwa tuhuma za kuhusika kwao na kashfa ya kampuni tata ya umeme ya Richmond, kama ilivyo kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, ambaye naye ameondolewa nafasi hiyo na Rais kwa maelezo kuwa anakwenda likizo ya kustaafu.

No comments: