Sunday, October 18, 2009

wabongo pia ni wacheshi!!!!!!!!!

Bongo kuna kina Mr Bean weengi 'Wachekeshaji' lakini kila mtu ana style yake ya uchekeshaji, huyu ye anakwambia anauwezo wa kuchekesha Ki Mr Bean vitendo bila kuongea na anaweza kwa vitendo na kulonga.
Ukipata nafasi ya kukaa na Mkwele dakika chache na kupiga naye stori unaweza kujiuliza hivi familia yake inaishi vipi naye? Si wanacheka kila saa?
Kijana huyo ana kila sifa anayotakiwa kuwa nayo mchekeshaji. Unapozungumza naye ana maneno mengi ya kuchekesha, ambayo muda wote utajikuta ukifurahi kumskiliza na kuangua kicheko.
Anaweza akakuangalia asizungumze lolote ukajikuta ukicheka tu kutokana na vitimbi vyake na jinsi anavyojibaraguza na kugeuzageuza macho na mdomo.
Mkwele ambaye ni nadhifu mno anapokuwa mitaani, anasema anaweza kuigiza vizuri zaidi vichekesho kuliko filamu.
Anasema katika filamu huwa hajisikii huru wala haoni kama anaziweza 'kufoji' au kujilazimisha. "Unajua kipaji changu mimi ni kuchekesha ndio maana mara nyingi unaniona nafanya komedi na ndio zilizoniweka kwenye chati kuliko filamu au maigizo mengine ya kawaida,"anasema.
"Komedi naimudu na naiweza kwani pamoja na kuigiza nina uwezo mkubwa wa kuitengeneza sura yangu na kuonekana kichekesho bila hata ya kuongea lolote.
"Fani ya uigizaji hasa ya komedi ni ngumu sana tofauti na watu wengine wanavyofikiria, inahitaji ubunifu wa hali ya juu ili kuikamata hadhira,"anasema Mkwele.
"Uigizaji wa kawaida pamoja na kuwa una ugumu lakini ni rahisi kwani utakapotakiwa uigize kama Baba, Hakimu, Mama mtu yeyote anaweza kufanya hivyo ilimradi awe na kipaji cha kuigiza tu.
"Lakini linapokuja suala la kuchekesha ni kipaji cha ziada usifanye masihara kubuni kitu kumfanya mtu acheke si kazi ndogo hata kidogo, ni kweli kabisa nimeshiriki katika filamu kama 'Cleopatra' na nyingine mbili lakini sioni kama ninafanya vizuri kama ninavyofanya kwenye Mizengwe."
"Unajua katika maisha, pamoja na kuwa kila mmoja wetu ana fani yake wakati mwingine si vibaya kujaribu kazi nyingine hasa katika kujitafutia riziki," anasema.
Akizungumzia wasanii anaowazimikia ndani na nje ya nchi Mkwele anasema wa ndani ni Binti Kiroboto na wasaanii wa nje ni Harrison Ford na Mr. Bean.
"Uchekeshaji kimataifa umekuwa na soko sana tofauti na hapa kwetu na hii ni kutokana na Watanzania wengi kutopenda kuthamini kazi za wenzao jambo linalotufanya tudumae.
"Lakini mipango yangu ya baadaye ni kuhakikisha kazi zangu zinafahamika kitaifa na kimataifa, si hivyo tu pia nimedhamiria kufanya kazi kwa bidii ili hadi kufikia mwaka 2012 panapo majaaliwa nianzishe kitu changu, inaweza kuwa kampuni studio au kitu chochote."anasema
Mkwele na kutoa wito kwa wasanii wote nchini waichukulia fani hiyo kama kazi na kuifanya kwa kujali miiko. "Kwa kufanya hivyo sanaa itafika mbali hata kama hatutawafikia kina Rambo lakini tutawakaribia."
"Ili ndoto za wasanii zifanikiwe serikali ina kazi kubwa ya kuwalinda wasanii kwa kutunga na kusimamia sheria zinazoangalia kazi za wasanii nchini," anasema.
Kuhusu uhusiano wa kimapenzi, Mkwele anasema ana mchumba na mtoto mmoja ingawa hakutaka kuzungumzia kiundani zaidi kwamba dada huyo ni yupi.
"Bado nazichanga ili nifunge ndoa na mchumba wangu, si unajua tena maisha yalivyoba kwa sasa?"anasema mchekeshaji huyo ambaye amekuwa kwenye chati hasa katika kikundi cha Mizengwe kinachorushwa na kituo cha televisheni ya ITV.
mambo safi bongo au siyo.hongera.

No comments: