Saturday, October 17, 2009

Watanzania wawili 'waula' taasisi za kimataifa

JAJI Bernad Luanda pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Godwin Ndossia wamechaguliwa kufanya kazi katika taasisi mbili tofauti za kimataifa.


Wakati Jaji Luanda amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa chama cha majaji na mahakimu wa Jumuiya ya Madola kanda za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini ya Afrika, Ndossi amechaguliwa kuwa mwakilishi wa Bara la Afrika kwenye kamati ya utendaji ya Shirikisho la Kimataifa linalojishughulisha na Sayansi ya Lishe Duniani (IUNS).

Jaji Luanda alichaguliwa hivi karibuni katika uchaguzi uliofanyika katika kongamano la mkutano mkuu wa majaji ulioketi katika visiwa vya Turks na Caicos vilivyopo Caribbean.

Taarifa iliyotolewa na Msajili wa Mahakama ya Rufaa nchini, Francis Mutungi, ilisema kongamano hilo liliwachagua pia Jaji Norma Wade Miller kutoka Bermuda (Kanda ya Caribbean ) kuwa Rais wa chama hicho.

Jaji Luanda ni Rais wa chama cha majaji na mahakimu cha Tanzania, pia makamu wa kwanza wa Rais wa chama cha majaji na mahakimu cha Afrika ya Mashariki.

Ndossi yeye alichaguliwa kwenye nafasihiyo katika mkutano wa IUNS uliofanyika kuanzia Oktoba 4 hadi 9, mwaka huu nchini Thailand.

Akizungumzia jijini Dar es Salaam juzi, Ndossi alisema ni mara ya kwanza kwa Mtanzania kuteuliwa kwenye nafasi ya kuwakilisha bara la Afrika katika taasisi hiyo nyeti ya IUNS ambayo hujadili masuala muhimu ya lishe duniani.

Lakini akasema ni changamoto kubwa kwake hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamesababisha ukame ambao umedumu kwa miaka miwili.

"Hali ya lishe kwa bara la Afrika ni mbaya sana. Ukame umaathiri uzalishaji wa chakula na kasi ya utapia mlo inaongezeka kwa kasi kubwa," alisema Ndossi.

Katika bara la Afrika, alisema nchi zinazokabiliwa na utapiamlo wa kutisha ni zile ambazo zinakabiliwa na machafuko ya muda mrefu ya vita kama vile Somalia na Sudan.

Utafiti uliofanywa na TFNC siku za karibuni, Ndossi alisema unaonyesha kwamba wilaya za Longodo mkoani Arusha na Nachingwea mkoani Mtwara, ndizo zilizokatika hali mbaya ya utapia mlo hapa nchini.

Katika utafiti huo ambao alisema unatarajia kutolewa na TFNC karibuni, wilaya nyingine ambazo nazo zinakabiliwa na tatizo hilo nchini pamoja na mikoa ilipo kwenye mabano ni Bagamoyo (Pwani), Same (Kilimanjaro), Ruangwa (Lindi), Kongwa (Dodoma), Monduli (Arusha) na Mufindi (Iringa).

Akielezea juu ya hali hiyo ya utapia mlo, Ndossi alisema wanawake na watoto ndio wanataabika kwa kiwango kikubwa na tatizo hilo.

Kuhusu vigezo vilivyotumika katika kupima tatizo hilo alisema: "Tulichunguza hali za afya za kinamama na watoto. Katika jamii hawa ni kama pima joto ya tatizo la utapiamlo," alisema mjumbe huyo wa Afrika IUNS.

mambo si ndo hayoo!!!je wabongo mnasemaje?sema maoni yako.

No comments: